window.__reverb = {}; window.__reverb.__reverbLoadedPromise = new Promise((resolve, reject) => { window.__reverb.__resolveReverbLoaded = resolve; window.__reverb.__rejectReverbLoaded = reject; }); window.__reverb.__reverbTimeout = setTimeout(() => { window.__reverb.__rejectReverbLoaded(); }, 5000);

Netanyahu: Jeshi litaingia Gaza 'kwa nguvu zake zote' katika siku zijazo

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jumanne kwamba jeshi la Israel litaendelea na operesheni zake katika Ukanda wa Gaza kwa "nguvu kamili" katika siku zijazo, akisisitiza kwamba vita havitakoma kwa sasa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara kwa leo, tukutane tena hapo kesho. .

  2. Serikali ya Uganda kulipatia jeshi mamlaka ya kuendesha kesi za raia?

    g

    Serikali ya Uganda iwasilisha rasmi muswada unaolenga kuipa mahakama ya kijeshi mamlaka ya kikatiba kusikiliza kesi dhidi ya raia wa kawaida.

    Mapema mwaka huu, Mahakama ya juu ya nchi hiyo ilitoa uamuzi na kupiga marufuku mahakama ya kijeshi dhidi ya kusikiliza kesi za raia.

    Muswada wa marekebisho juu ya sheria ya jeshi la UPDF wa mwaka 2025, kwa mara ya kwanza umesomwa leo bungeni Juma nne (Mei 13) na waziri wa ulinzi wa Uganda Jacob Oboth Oboth.

    Muswada huo wenye kurasa 144, unanuia kufanya marekebisho katika sheria ya jeshi la UPDF iliopitishwa mwaka 2005 na unalenga kuhalalisha mahakama ya kijeshi katika kusikiliza kesi dhidi ya raia wa kawaida ambao watapatikana na silaha kinyume na sheria.

    Itakumbukwa kuwa Januari 31, jopo la mahakimu saba likiongozwa na hakimu mkuu wa Uganda Alfonse Owiny-Dollo lilitoa uamuzi wa kihistoria na kufutilia mbali mahakama za kijeshi nchini Uganda, huku ikiamrisha kesi zote za raia wa kawaida katika mahakama hizo kuhamishwa hadi mahakama za kiraia.

    Uamuzi huo unakuja wakati mwanasia mkongwe wa upinzani nchini Uganda Dkt Kizza Besigye akikabiliwa na kesi katika mahakama ya kijeshi, lakini kufuatia uamuzi huo, kesi yake ilihamishiwa katika mahakama ya kiraia ambako alifunguliwa mashtaka ya uhaini.

    Katika baadhi ya mapendekezo kwenye muswada huo, ni kwamba mtu yeyote atakayepatikana, kumiliki au kuuza sare ya jeshi bila idhini atapaswa kufikishwa katika mahakama ya kijeshi. Lakini baadhi ya raia na watetezi wa haki za kibinadamu wamekosoa hatua ya kutaka kurejesha tena mahakama za kijeshi hasa baada ya muhimili wa sheria kuzipiga marufuku.

    Kuhusu vigezo vya mwenyekiti wa mahakama ya kijeshi, muswada huo unapendekeza kiongozi wa mahakama hiyo aliyehitimu kwa kiwango cha shahada katika masuala ya sheria, asiye chini ya cheo cha Kapteni na ambaye amehudumu kwa angalu miaka mitatu.

    Baada ya kusomwa bungeni, muswada huo umewasilishwa kwa kamati ya ulinzi na mambo ya ndani bungeni ambako utafanyiwa ukaguzi na kamati hiyo kutoa ripoti yake juu ya muswada huo wakati wa kusomwa bungeni kwa mara ya pili.

  3. Marekani na Saudi Arabia zatia saini mkataba wa silaha wa $142bn

    Trum na MBS

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman wametia saini mkataba wa silaha wa thamani ya dola bilioni 142 katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kidiplomasia.

    Mkataba huo uliofikiwa kati ya Marekani na Saudi Arabia unatajwa kuwa "makubaliano makubwa zaidi ya mauzo ya ulinzi katika historia", Ikulu ya Marekani inasema.

    Marekani aidha inasema mkataba huo utaiwezesha Saudi Arabia kupata ''silaha za kisasa za kivita''.

    Katika taarifa kwa vyombo vya habari ya White House, Marekani inasema mauzo ya silaha yanajumuisha makundi matano ikiwa ni pamoja na:

    • Kuimarisha uwezo wa jeshi la anga
    • Ulinzi wa anga
    • Makombora ya Usalama wa baharini na pwani
    • Usalama wa mipaka na uboreshaji wa vikosi vya ardhini
    • Uboreshaji wa mifumo ya habari na mawasiliano
  4. Netanyahu: Jeshi litaingia Gaza 'kwa nguvu zake zote' katika siku zijazo

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jumanne kwamba jeshi la Israel litaendelea na operesheni zake katika Ukanda wa Gaza kwa "nguvu kamili" katika siku zijazo, akisisitiza kwamba vita havitakoma kwa sasa.

    Netanyahu alithibitisha kuwa Israel inajitahidi kutafuta nchi zinazoweza kuwapokea wakazi wa Gaza, akidokeza kuhusu juhudi zinazowezekana za kuwapa makazi baadhi ya wakaazi wa Ukanda huo nje ya maeneo ya Palestina.

    Aliongeza kusema kuwa , "Sioni hali ambayo Israel itasimamisha vita hivi sasa. Tutaendelea hadi tutimize malengo yetu ya usalama."

    Mapema Jumanne asubuhi, jeshi la Israel lilitangaza kuwa limeshambulia kwa mabomu "kituo cha kuamrisha na kudhibiti" cha Hamas ndani ya hospitali moja huko Gaza, ambayo harakati hiyo ilikuwa ikitumia kutekeleza "shughuli za kigaidi," kama ilivyosema.

    Jeshi lilisema katika chapisho kwenye Telegram kwamba "lililipua kwa usahihi kituo cha amri za jeshi na udhibiti kilichoko ndani ya Hospitali ya Nasser huko Khan Yunis," kusini mwa Ukanda wa Gaza.

    Unaweza pia kusoma:

  5. Jeshi la Polisi Tanzania lathibitisha kumkamata Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara

    X

    Na Humprey Mgonja

    BBC Dar es Salaam

    Taarifa kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inaeleza kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Amani Golugwa, alikamatwa na jeshi hilo majira ya saa sita usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akiwa katika maandalizi ya kusafiri kuelekea Brussels, Ubelgiji.

    Jeshi la Polisi linadai kuwa sababu ya kumkamata Golugwa ni kutokana na taarifa za siri walizonazo, ambazo zinahusisha mienendo yake ya kuondoka na kurudi nchini bila kufuata taratibu za kisheria zinazotakiwa.

    "Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu suala hili, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama," imeeleza taarifa hiyo.

    Hapo awali, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilitoa taarifa ikieleza kuwa kiongozi wao alikamatwa akiwa anaelekea Ubelgiji kwa ajili ya kuwakilisha chama katika Mkutano wa International Democracy Union (IDU) unaoanza kesho nchini humo. Taarifa ya chama hiyo inasema kuwa tayari wamewatuma mawakili wao polisi kutoa usaidizi wa kisheria kwa kiongozi wao.

    Kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za International Democracy Union (IDU), wamelaani kukamatwa kwa Golugwa, wakidai kuwa ni hatua ya kunyamazisha upinzani na kumtaka aachiliwe mara moja kwani ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

  6. Kampeni za uchaguzi zaanza rasmi Burundi

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kwa kipindi cha wiki tatu kuanzia Jumanne hii, tarehe 13 Mei , 2025 vyama vya siasa na watu huru vinazunguka maeneo mbalimbali nchini kuwaomba wananchi wawapigie kura katika uchaguzi wa tarehe 5 Juni.

    Kutakuwa na uchaguzi wa wabunge, maseneta na madiwani wa manispaa.

    Mwaka huu, hakutakuwa na uchaguzi wa rais, tofauti na uchaguzi wa tangu 2005, kwasababu kuanzia 2020 muhula wa urais utakuwa miaka saba. Uchaguzi ujao wa urais utafanyika mwaka wa 2027.

    Lakini wapo waliokwenda kwenye kampeni na kulalamika.

    Kulingana na takwimu zilizotolewa na Tume ya taifa ya uchaguzi CENI, jumla ya Warundi 6,013,498 walijiandikisha kupiga kura.

  7. Walioachwa bila makazi duniani waongezeka maradufu

    XX

    Chanzo cha picha, AFP

    Takwimu mpya zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni themanini sasa wameachwa bila ya makazi ulimwenguni,ikiwa idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.

    Takwimu hizo zilizochapishwa na shirika la kimataifa la kutoa misaada ya kiutu la Norwegian Refugee Council NRC na kituo cha kufuatilia matukio yanayosababisha watu kulazimika kuyahama makazi yao IDMC,zinaonesha idadi ya watu walioathirika imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

    Ripoti hiyo inasema watu wasiopungua milioni 74 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mizozo na ghasia. Asilimia tisini kati ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao ni kutokana na vita na mizozo.

    Katika ukanda wa Gaza huko Palestina karibu kila mtu aliachwa bila ya makazi kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita. Wapalestina wa Gaza zaidi ya milioni mbili wameachwa bila ya makazi kutokana na mashambulizi makali ya mara kwa mara kutoka kwa Israel.

    Sudan ina zaidi ya watu milioni 11 walioachwa bila ya makazi,ikiwa idadi kubwa zaidi kurekodiwa katika taifa moja.

    Nchi nyingine zilizotajwa mwenye ripoti hiyo ambazo zina idadi kubwa ya watu walioachwa bila ya makazi ndani ya nchi zao ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,Chad na Afghanistan.

    Sababu nyingine zilizosababisha watu kuachwa bila ya makazi ni umasini na mabadiliko ya tabia nchi.

    Majanga yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha takriban watu milioni 45 kuyahama makazi yao.

  8. Mahakama ya Kenya yaamuru Mbunge wa zamani wa Afghanistan kurejeshwa Marekani

    Mahakama nchini Kenya imeidhinisha kurejeshwa nchini Marekani kwa aliyekuwa mbunge wa Afghanistan Haji Abdul Zaher Qadir.

    Bwana Qadir anakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kuingiza dawa za kulevya na kumiliki bunduki nchini humo.

    Hakimu Mkuu Mwandamizi Ben Mark Ekhubi alisema ombi la kurejeshwa lilihalalishwa na akaamuru Qadir ikabidhiwe kwa mamlaka ya Marekani.

    Qadir alikamatwa jiji Nairobi baada ya kuwasili nchini kutoka Kabul na amekuwa akishikiliwa na mamlaka tangu wakati huo.

    Marekani ilitoa waranti ya kukamatwa kwake mwezi Machi 2025. Hata hivyo Qadir anakanusha mashtaka na anasema kesi hiyo inachochewa na msukumo wa kisiasa.

    Wakili wake alisema mahakama ilipuuza hoja muhimu za utetezi na itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

    Qadir atazuiliwa gerezani huku rufaa ikisikilizwa. Rufaa yake ikikataliwa atapelekwa Marekani ndani ya siku 15.

  9. Mwanahabari wa Gaza Hassan Aslih auawa katika shambulio Israel

    Hassan Aslih alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Nasser alipouawa katika shambulio la anga

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Hassan Aslih alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Nasser alipouawa katika shambulio la anga

    Mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza yamesababisha kifo cha mwanahabari mashuhuri wa Kipalestina, duru za matibabu na mashuhuda wa tukio hilo wamesema.

    Hassan Aslih, ambaye alikuwa akitibiwa majeraha ya shambulio la awali la Israel, alilengwa katika kile mashahidi walieleza kuwa ni shambulio la ndege isiyo na rubani katika kitengo cha upasuaji cha hospitali hiyo.

    Daktari wa hospitali hiyo amethibitisha kuwa Aslih alikuwa amelazwa kwa karibu mwezi mmoja baada ya kunusurika shambulio la anga dhidi ya kituo hicho cha afya mwezi Aprili.

    Jeshi la Israel hapo awali lilimshutumu Aslih kwa kuhusika katika shambulio la Oktoba 7 la Hamas dhidi ya Israel.

    Waandishi kadhaa walijeruhiw katika shambulio la Israel la mwezi Aprili.

    Soma zaidi:

  10. Duterte ashinda uchaguzi wa meya akiwa The Hague

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte amechaguliwa tena kuwa meya wa jiji la Davao, licha ya kufungwa huko The Hague kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu.

    Kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa, Duterte, 80, aliongoza kwa takriban kura 405,000 - mbele ya mshindani wake wa karibu aliyefuata 49,000, kulingana na matokeo yasiyo rasmi kutoka kwa tume ya uchaguzi iliyochapishwa na vyombo vya habari vya eneo.

    Duterte alikamatwa na kusafirishwa kwa ndege hadi The Hague mwezi Machi kutokana na kile alichokiita "vita dhidi ya dawa za kulevya", ambapo maelfu ya watu waliuawa kwa kupigwa risasi mitaani.

    Lakini licha ya madai hayo ambayo Duterte amekanusha - wachambuzi wamesema kukamatwa kwake kumezidisha uungwaji mkono kwake na familia yake.

  11. Wafanyakazi wa nyumbani Saudi Arabia wanapitia unyanyasaji - Amnesty International

    .

    Chanzo cha picha, Amnesty

    Shirika la Amnesty International limesema kuwa wanawake wa Kenya ambao huajiriwa kufanya kazi za nyumbani nchini Saudi Arabia hulazimika kuvumilia mazingira ya kazi ambayo ni ya kikatili na kibaguzi.

    "Mazingira haya yanaweza kufananishwa na kazi ya kulazimishwa na ulanguzi wa watu," Amnesty International imesema.

    Ripoti hiyo inaangazia namna waajiri wanavyowanyanyasa wanawake hawa majumbani mwao kutokana na mitazamo ya ubaguzi wa rangi, na namna wafanyakazi wa nyumbani wanavyotengwa na sheria ya kazi na mageuzi yanayohusiana na kazi nchini Saudi Arabia.

    Amnesty International inasema mara nyingi wanaowatafutia kazi wanawake hawa huwadanganya kuhusu hali ya kazi watakazofanya lakini wanapofika Saudi Arabia wanalalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu sana.

    "Wengine wanabakwa, wanatukanwa na kupigwa. Waajiri wanachukua pasipoti na simu zao na wakati mwingine wanakataa kuwalipa mishahara, Wanawake hawa walienda Saudi Arabia kutafuta kazi ili wasaidie familia zao lakini wakajipata wakivumilia mateso makali majumbani mwa waajiri wao", amesema Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya.

    "Nilihisi kama mtu aliyenaswa kwenye mtego wakati nikiwa Saudi Arabia," alisema Joy ambaye alifanya kazi nchini Saudi Arabia.

    "Sina uhuru wowote kwa sababu unapoingia, huwezi kutoka. Hutoki wala huoni nje." Hii ilinifanya nihisi kana kwamba niko gerezani," Joy aliongeza.

    Saudi Arabia imeanzisha mageuzi machache katika mfumo wa kafala unaowaweka wafanyakazi chini ya udhibiti wa waajiri wao lakini bado wafanyakazi wa nyumbani wanawekewa masharti makali.

    Amnesty International inasema Saudi Arabia kuna takriban Wakenya 150,000 wa kazi za nyumbani.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Habari za hivi punde, Air Force One yatua Saudi Arabia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ndege ya rais Donald Trump, Air Force One, imetua hivi punde nchini Saudi Arabia, na kuanza ziara ya kwanza kuu ya kimataifa ya rais huyo wa Marekani katika muhula wake wa pili.

    Mkutano wa awali kati ya viongozi wa Marekani na Saudi Arabia umeanza

    Donald Trump na Mwanamfalme Mohammed bin Salman wamekutana katika mkutano wa kwanza.

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio pia yuko kwenye mkutano huo.

  13. Waasi wa Houthi wamekubali kuachana na mapigano - Trump

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Oman ilitangaza wiki iliyopita kuwa imeanzisha mapatano kati ya Marekani na waasi wa Houthi nchini Yemen kufuatia wiki saba za mazungumzo.

    Trump alisema wiki iliyopita kwamba waasi wamekubali kuachana na mapigano.

    "[Wahouthi] hawataki kupigana, tutaheshimu hilo na tutasitisha mashambulizi ya mabomu, na wamesalimu amri," alisema.

    Tangu Novemba 2023, Wahouthi - kundi la waasi wanaoungwa mkono na Iran wanaodhibiti sehemu kubwa ya Yemen - wamekuwa wakishambulia meli katika Bahari ya Shamu wakionyesha kuunga mkono Wapalestina huko Gaza.

    Chini ya Rais wa zamani Joe Biden Marekani ilianzisha mashambulizi dhidi ya waasi, ambayo yameongezeka chini ya Trump.

    Jeshi la anga la Uingereza pia limefanya mashambulizi katika wiki za hivi karibuni.

    Wahouthi waliwahi kusema kuwa Marekani ilibadili msimamo wake na kwamba makubaliano hayo hayajumuishi makubaliano ya kukomesha mashambulizi dhidi ya Israel.

    Soma zaidi:

  14. Rapa Tory Lanez akimbizwa hospitalini baada ya kudungwa kisu mara 14 katika gereza la California

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Msanii huyo wa muziki wa hip-hop wa Canada alishambuliwa na mfungwa mwingine Jumanne asubuhi katika Taasisi ya Kurekebisha Tabia ya California huko Tehachapi, takriban maili 75 (120km) kaskazini mwa Los Angeles, maafisa wa gereza waliambia BBC.

    Rapa huyo mwenye umri wa miaka 32 alipata majeraha mwilini - na kusababisha mapafu yake kushindwa kufanyakazi, kulingana na ujumbe kwenye akaunti yake ya Instagram.

    Lanez, ambaye jina lake asili ni Daystar Peterson, anatumikia kifungo cha miaka 10 jela kwa kumpiga risasi mwanamuziki mwenzake Megan Thee Stallion mnamo mwaka 2020.

    Ujumbe kwenye ukurasa wa Instagram wa nyota huyo ulisema alichomwa kisu mgongoni, kwenye kiwiliwili, kichwani na usoni. Aliwekwa kwa muda kwenye kifaa cha kupumua lakini sasa anaweza kupumua mwenyewe, ujumbe kwenye Instagram uliongeza.

    "Licha ya kuwa na uchungu, anazungumza kama kawaida, na anamshukuru Mungu sana kwamba bado yuko hai," ujumbe huo ulisema.

    Wafanyakazi wa magereza walianza huduma ya kwanza kabla ya Lanez kupelekwa katika kituo cha matibabu cha eneo hilo kwa matibabu zaidi, alisema.

    Uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo la kuchomwa kisu, Bw Calderón Michel aliambia BBC. Hakuzungumzia nia ya mshambuliaji huyo.

    Lanez alihukumiwa mwaka wa 2023 kwa mashtaka matatu ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kushambulia kwa kutumia bunduki.

    Alimpiga risasi Megan Thee Stallion, ambaye jina lake asili ni Megan Pete, walipokuwa wakitoka kwenye tafrija katika jumba la nyota wa kipindi cha TV Kylie Jenner.

    Wawili hao waligombana ndani ya gari kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi na kazi zao kitaaluma, Megan Thee Stallion alisema hayo wakati anatoa ushahidi katika kesi hiyo.

    Alisema alitaka amruhusu kutoka ndani ya gari, na hapo ndipo Lanez alipoanza kufyatua risasi chini na kumfokea huku akimwambia "cheza".

    Alihitaji kufanyiwa upasuaji ili kuondoa vipande vya risasi kwenye mguu wake.

    Lanez alikataa kuomba msamaha na alidumisha kutokuwa na hatia katika tukio hilo la upigaji risasi.

  15. Waafrika Kusini walio wazungu wawasili Marekani chini ya Mpango wa Wakimbizi wa Trump

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kundi la Wazungu 59 wa Afrika Kusini wamewasili Marekani, ambapo watapewa hadhi ya ukimbizi.

    Rais Donald Trump amesema maombi ya wakimbizi kwa Waafrika na walio wachache nchini humo yameharakishwa kwa sababu walikuwa waathiriwa wa "ubaguzi wa rangi".

    Serikali ya Afrika Kusini ilisema kundi hilo halipitii mateso yoyote ambayo yangestahili hadhi ya ukimbizi.

    Utawala wa Trump umesitisha uandikishaji mwingine wote wa wakimbizi, pamoja na waombaji wengine kutoka maeneo yenye vita.

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilielezea hatua hiyo kama badiliko la kikatili la ubaguzi wa rangi, likisema kuwa maelfu ya watu - wengi wao ni wakimbizi waafrika na wa Afghanistan - wamenyimwa hifadhi hiyo nchini Marekani.

    Kundi la Wazungu Waafrika Kusini, ambao walitua katika uwanja wa ndege wa Dulles karibu na Washington DC siku ya Jumatatu, walipokelewa vizuri na mamlaka ya Marekani.

    Wengine walishika watoto wadogo na kupeperusha bendera ndogo za Marekani katika eneo walilokuwa wamewasili.

    Mchakato wa kupata hadhi ya ukimbizi nchini Marekani mara nyingi huchukua miezi na hata miaka, lakini kundi hili limefuatiliwa haraka.

    UNHCR - shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi - lilithibitisha kwa BBC kuwa halikuhusika katika mchakato wa uhakiki kama ilivyo kawaida.

    Alipoulizwa moja kwa moja siku ya Jumatatu kwa nini maombi ya wakimbizi wa Afrika wenye asili ya wazungu yameshughulikiwa haraka kuliko makundi mengine, Trump alisema "mauaji ya halaiki" yalikuwa yanafanyika na kwamba "wakulima wenye asili ya kizungu" walikuwa wakilengwa.

    "Wakulima wazungu wanauawa, lakini ama wawe ni wazungu au waafrika hakuna tofauti yoyote kwangu."

    Soma zaidi:

  16. Raia wa Marekani na Israel aungana tena na familia yake baada ya kuachiliwa na Hamas

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mateka wa Israel na Marekani Edan Alexander ameungana tena na familia yake nchini Israel baada ya kushikiliwa na Hamas huko Gaza kwa muda wa miezi 19.

    Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 21 alikuwa akitumikia jeshi la Israel kwenye mpaka wa Gaza alipotekwa na wanamgambo wa Hamas tarehe 7 Oktoba.

    Siku ya Jumatatu, Israel ilisitisha operesheni zake za kijeshi huko Gaza kwa saa chache ili kuwezesha uhamisho huo.

    Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas aliiambia BBC kuwa kutolewa kwake kulikusudiwa kuonyesha ishara ya nia njema na kama sehemu ya juhudi za kufikia makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kabla ya ziara ya Rais wa Marekani Donald Trump katika Mashariki ya Kati siku ya Jumanne.

    Bw Alexander anadhaniwa kuwa raia wa mwisho wa Marekani anayeshikiliwa na Hamas ambaye bado alikuwa hai.

    Katika taarifa, familia yake ilimshukuru rais wa Marekani lakini pia iliitaka serikali ya Israel na wapatanishi kuendeleza juhudi zaidi ili kuwakomboa mateka 58 waliosalia.

    Bw Alexander ndiye mateka wa kwanza kuachiliwa na Hamas tangu Israel ianze tena mashambulizi yake ya kijeshi tarehe 18 Machi, baada ya kumalizika kwa muda wa miezi miwili wa kusitisha mapigano.

    Soma zaidi:

  17. Diddy alitumia umaarufu wake kuwadhulumu na kunyanyasa wanawake - waendesha mashtaka

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Bw Combs na Cassandra Ventura pichani mnamo 2017

    Sean "Diddy" Combs alitumia umaarufu na vurugu kuwanyanyasa kingono wanawake, waendesha mashtaka wamesema katika ufunguzi wa taarifa ya kesi ya mwanamuziki huyo, huku mawakili wake wakitetea maisha yake ya kujihusisha na "ngono za ovyoovyo".

    "Diddy" Combs mwenye umri wa miaka 55 amekanusha mashtaka yakiwemo ya ulaghai, ulanguzi wa ngono na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba.

    Mahakama pia ilisikiza kutoka kwa mashahidi wa kwanza wa waendesha mashtaka, akiwemo mlinzi wa hoteli ambapo Bw Combs anaonekana kwenye video ambayo sasa ipo mtandaoni akimpiga mpenzi wake wa zamani mwaka wa 2016.

    Ushahidi wake ulifuatiwa na mwanamume aliyesema Bw Combs alimdhulumu mpenzi wake wa zamani wakati wa kufanya ngono za kulipwa na wanandoa hao.

    Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuona ni ya kuhuzunisha.

    Baada ya kuketi kwa jopo la majaji 12 na wengine sita waliokuwa mbadala siku ya Jumatatu asubuhi, serikali na mawakili wa Bw Combs walielezea kesi zao.

    Mwendesha mashtaka Emily Johnson alimshutumu Bw Combs kwa kutumia hadhi yake ya mtu mashuhuri na mzunguko wa wandani wa wafanyikazi "waaminifu" kuwanyanyasa wanawake kingono na kuendesha biashara ya uhalifu.

    Alilenga waathiriwa wawili katika kesi hiyo - mpenzi wa zamani wa Bw Combs, Cassandra Ventura, na mpenzi mwingine wa zamani ambaye jina halikutajwa.

    Waendesha mashitaka waliambia mahakama kwamba Bw Combs alitumia vurugu na kutishia taaluma ya muziki ya Bi Ventura ili kumlazimisha kufanya ngono zisizo za ridhaa na kufanya vitendo vya ngono na wanaume wengine wakati wa kile kinachojulikana kama "freak-offs" iliyorekodiwa na Bw Combs.

    Mshtakiwa "alikuwa na uwezo wa kuharibu maisha yake [Bi Ventura]," Bi Johnson alisema.

    Kiini cha kesi hiyo ni video inayoonyesha Bw Combs akimpiga Bi Ventura na pia kumburuta nywele katika barabara ya ukumbi wa hoteli ya Los Angeles mnamo 2016.

    Wanasheria wa Bw Combs walisema kuwa video hiyo ilikuwa ushahidi wa tabia ya Bw Combs "yenye kasoro", lakini si ya biashara kubwa ya uhalifu. "Unyanyasaji wa majumbani sio biashara ya ngono," alisema Teny Geragos, wakili wa Bw Combs.

    Miongoni mwa waliotoa ushahidi ni pamoja na Daniel Phillip, meneja wa zamani wa watumbuizaji wa kiume wakiwa uchi, ambaye alisema alikutana na Bw Combs na Bi Ventura baada ya mkuu wake kumtaka awe kama mtumbuizaji mwenye kusherehesha wengine katika tafrija ya bachelorette.

    Lakini, Bw Phillip alisema, badala yake alipokelewa katika hoteli na Bi Ventura, ambaye alimwambia ilikuwa siku yake ya kuzaliwa na mumewe alitaka kumpa zawadi.

    Bw Phillip aliiambia mahakama kwamba aliendelea kufanya mapenzi na Bi Ventura mara kadhaa – kwa takriban muda wa saa 10, wakati mwingine chini ya ushawishi wa dawa za kulevya - huku Bw Combs akitazama na kurekodi tukio hilo.

    Alidai kuwa alishuhudia Bw Combs akimshambulia Bi Ventura angalau mara mbili, ikiwa ni pamoja na wakati mmoja alipomvuta nywele huku akiwa anapiga mayowe akisema "Samahani".

    Bwana Combs kisha akarudi chumbani pamoja na Bi Ventura na kuwataka wawili hao wafanye ngono tena mbele yake, Bw Phillip alisema.

    "Nilishtuka," alisema. "… Niliogopa sana."

    Bw Phillip alidai kwamba hakuripoti tukio hilo polisi kwa kuhofia kuwa Bw Combs ni "mtu mwenye uwezo mkubwa" na kwamba anaweza "kukuua".

    Kesi hiyo imeratibiwa kuendelea Jumanne wakati Bi Ventura anatarajiwa kutoa ushahidi wake.

    Soma zaidi:

  18. Urusi ilidungua ndege ya Malaysia Airlines, MH17 - shirika la UN

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi ilidungua ndege ya Malaysia Airlines, MH17, mashariki mwa Ukraine mnamo Julai 2014, shirika la Umoja wa Mataifa la usafiri wa anga limesema.

    Watu wote 298 waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya abiria walifariki dunia ndege hiyo ilipodunguliwa na kombora lililotengenezwa Urusi.

    Kremlin daima imekuwa ikikanusha kuhusika na ajali hiyo.

    Siku ya Jumatatu, Baraza la Umoja wa Mataifa la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) lilipiga kura na kuamua kwamba Urusi ilishindwa kutekeleza majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa ya anga, ambayo inazitaka nchi "kujizuia kutumia silaha dhidi ya ndege za kiraia zilizoangani".

    Ndege ya shirika la ndege la Malaysia MH17 ilikuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur ilipoanguka katika eneo la Donbas nchini Ukraine, wakati wa mzozo kati ya waasi wanaoiunga mkono Urusi na wanajeshi wa Ukraine.

    Wengi wa abiria na wafanyakazi,196, walikuwa wanatoka Uholanzi.

    Pia kulikuwa na watu 38 kutoka Australia, raia 10 wa Uingereza, pamoja na raia wa Ubelgiji na Malaysia.

    Kesi hiyo kwa Umoja wa Mataifa iliwasilishwa mwaka 2022 na serikali za Australia na Uholanzi, ambazo zote zimefurahishwa na uamuzi huo.

    "Tunatoa wito kwa Urusi hatimaye kukabiliana na wajibu wake kwa kitendo hiki cha kutisha cha vurugu na kulipa fidia kwa tabia yake mbaya", alisema waziri wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong katika taarifa.

    Mnamo 2022, mahakama ya Uholanzi ilitoa uamuzi wa kwamba kikundi kinachodhibitiwa na Urusi kiliangusha ndege hiyo na Warusi wawili na raia wa Ukraine anayeunga mkono Moscow walipatikana na hatia ya mauaji bila kuwepo.

    Watatu hao wote walihukumiwa kifungo cha maisha jela, hata hivyo, kwa kuwa hawakurudishwa, hawajatumikia kifungo.

    Soma zaidi:

  19. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 13/05/2025.