Jinsi mchakato wa kuwarudisha mateka wa Israel nyumbani kutoka Gaza unavyofanyika

Chanzo cha picha, Reuters
Huanza na simu inayoelezea eneo.
Mara baada ya maelezo kupokelewa, timu kutoka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) inaondoka kwa magari yenye nembo ya shirika la kibinadamu ili kuwachukua mateka huko Gaza.
Wanajeshi wa Israeli na wafanyakazi wa kitabibu pia wamekusanyika katika maeneo kadhaa tofauti, wakingojea kuwarudisha nyumbani.
Kuachiliwa kwa mateka, kunatazamwa kote ulimwenguni, kumekuja baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo ya mvutano yenye lengo la kumaliza vita vilivyoanza tarehe 7 Oktoba 2023, wakati wapiganaji wa Hamas walipowaua takribani watu 1,200 nchini Israel na kuwateka nyara wengine 251.
Katika miezi 15 iliyofuata, zaidi ya Wapalestina 47,000 waliuawa huko Gaza, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, na wengi zaidi walipoteza makazi yao katika mashambulizi ya Israel.
Chini ya masharti ya mkataba wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas ulioanza tarehe 19 Januari, jumla ya mateka 33 wa Israel wanastahili kuachiliwa na kurejeshwa kwa familia zao wakati wa awamu ya kwanza, itakayodumu kwa wiki sita.
Kwa kubadilishana, mamia ya wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel wanaachiliwa huru.
Ikiwa chochote kitaenda vibaya, inahatarisha mateka kubaki utumwani, na vita kutawala.
"Hii ni zaidi ya kuendesha gari," anasema msemaji wa ICRC Sarah Davies.
"Operesheni hizi zinaweza kuonekana rahisi, lakini kwa kweli ni ngumu sana na zinahitaji hatua kali za usalama ili kupunguza hatari kwa wale wanaohusika."
ICRC, ambayo hufanya kazi kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote katika makabidhiano, hukusanya timu ya wataalamu, ambao baadhi yao wamehusika katika shughuli kama hizo hapo awali, ingawa hii ni changamoto zaidi.
Mipango muhimu
Kuna baadhi ya maelezo ambayo kundi hilo haliwezi kuzungumzia hadharani kwa sababu ya wasiwasi kwamba linaweza kuhatarisha usalama wa operesheni hiyo.
Bi Davies anasema kupanga ni muhimu ili kuhakikisha kuwa mabadilishano yanakwenda sawa. Wamepanga njia mbadala za kufikia maeneo tofauti huko Gaza, wakijua kwamba "njia salama inaweza kubadilika" wakati wowote.
Miongoni mwa mahangaiko yao makubwa ni hatari zinazoletwa na silaha zisizolipuka, miundombinu iliyoharibiwa, na umati mkubwa wa watu wenye "hisia zilizoongezeka".
"Timu zetu hujiandaa na kupanga matukio mengi iwezekanavyo," anasema.
"Jambo muhimu zaidi kwetu ni kuweza kumrudisha nyumbani akiwa salama mtu yeyote aliyekabidhiwa chini ya uangalizi wetu."
Lakini haiwezekani kupanga kwa kila kitu.
"Kutokana na uzoefu wa awali, hapa na katika maeneo mengine duniani kote, tunajua kwamba vifaa na maelezo ya mwisho yanaweza kubadilika wakati wowote, hata wakati wa operesheni yenyewe," anasema Bi Davies.
Wafanyakazi wa matibabu na wanaoitwa wataalamu wa uchafuzi wa silaha, waliofunzwa kutambua mabaki ya vita vya kulipuka, husafiri na timu.
Wakati wa operesheni, wawakilishi wa ICRC pia wanawasiliana mara kwa mara na maafisa wa Israeli na Hamas, pamoja na wapatanishi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika matukio ya awali ya kuachiwa wafungwa, Hamas ilisambaza majina ya mateka walioachiliwa mapema kwenye chaneli zake za Telegram, bila kufichua ni wapi makabidhiano yatafanyika.
Ishara za kwanza za hadhara za maeneo hayo ni uwepo wa wapiganaji wenye silaha na waliojifunika nyuso wa tawi la kijeshi la Hamas.
"Niligundua kutoka kwa kijana wa kioski kwamba kulikuwa na kitu kinachotokea kwenye makutano na kwamba wapiganaji wa al-Qassam walikuwa na gwaride," mwandishi wa habari wa ndani anasema kuhusu kutolewa kwa mara ya kwanza katika Jiji la Gaza mapema mwezi huu.
Umati wa watu ulianza kukusanyika kutazama wapiganaji hao wakikusanyika kwa mpangilio, na habari zikaanza kuenea kwamba mateka watatu wa kwanza walioachiliwa chini ya mpango wa kusitisha mapigano wangetokea huko.
"Wakati watu walipogundua kuwa hapa pangekuwa mahali ambapo wangewakabidhi mateka wa Israel, watu walianza kuimba [kwa ajili ya al-Qassam na viongozi wakuu wa Hamas]," anasema. "Walianza kupaza sauti 'Mungu ni mkuu zaidi' , hiyo ilionesha jinsi walivyokuwa na furaha."
Mwandishi huyo pia alikuwepo kwa ajili ya kuachiliwa kwa mara ya pili, katika eneo tofauti katika Jiji la Gaza, wiki iliyofuata, ambayo anaelezea kuwa "iliyojipangwa zaidi".
Wapiganaji waliweka eneo dogo la jukwaa na dawati na viti, na kusimama kwa mpangilio ili kuwatenganisha mateka na umati.
Magari meupe yenye madirisha meusi yalitumiwa kuwaleta mateka, askari wanne wanawake, kwenye eneo hilo.
Vijana hao wa kike walirekodiwa wakiwashukuru waliowateka na kukabidhiwa mikoba ya zawadi katika video iliyochapishwa na tawi la kijeshi la Hamas.
Walipandishwa jukwaani na kuwapungia mkono umati uliokuwa ukishangilia, kabla ya kukabidhiwa kwa ICRC.

Chanzo cha picha, Getty Images
Msemaji wa Hamas Abdul Latif al-Qanou alisema katika taarifa yake ya baadaye kwamba "mandhari na maelezo" ya makabidhiano hayo "yanasimulia hadithi ya ubunifu wa upinzani, ushujaa, na kuimarisha kielelezo cha fahari na utu".
Bi Davies anasema kuna baadhi ya vipengele vya makabidhiano ambavyo "viko nje ya uwezo wetu".
"Wakati wote, wafanyakazi wa ICRC hufanya kila wawezalo kulinda utu wa wale wanaoachiliwa, lakini ... ni muhimu kwamba watu watambue mapungufu ya kile tunachoweza kufanya," anasema.
"Kipaumbele chetu kinasalia kuwa kutolewa salama na kwa mafanikio na uhamisho wa wale walio chini ya uangalizi wetu."
Mateka hao wamehamishiwa kwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) nje kidogo ya Gaza.
Kanali Dk Avi Banov, naibu mkuu wa kikosi cha matibabu cha Jeshi la Ulinzi la Israel, anasema: "Tumejiandaa kupitia viunga vya Gaza na maeneo mengine kuwapokea mateka.
"Siku zote tunajiandaa kwa sababu Hamas hawatuambii, 'Sawa, tutawaweka huru katika eneo hili au katika eneo hilo'."
Katika mpaka, vituo vya kupokea vimewekwa ili kuwapokea.
Kwenye eneo hili kuna wanajeshi na wafanyakazi wa matibabu, wafanyakazi wa kijamii na familia za mateka.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, Getty Images
Daktari wa zamani wa jeshi la Israeli ambaye alihusika katika operesheni ya kwanza ya kuwarudisha mateka wakati wa usitishaji mapigano Novemba 2023 anakumbuka akisubiri karibu na gari la wagonjwa kwenye kituo karibu na mpaka.
Yake ilikuwa moja ya timu kadhaa zilizosimama ikiwa mmoja wa mateka alikuwa na dharura ya matibabu na anasema kulikuwa na maagizo madhubuti ya jinsi ya kuingiliana na wale waliorudi.
Anakumbuka: "Tuliambiwa ukiwahamisha usiwaulize maswali, usifanye jambo lisilofaa, nyamaza tu halafu mateka wakikuuliza kitu au wanataka kitu, bila shaka utajibu. wapeni."
Anasema hali katika eneo hilo ilikuwa ya msisimko, "Ilikuwa misheni muhimu sana," anasema.
Kanali Dkt Banov anasema kurudi kwao kunaanza na kutambulishwa kati ya mateka na wafanyakazi wa matibabu.
Mateka waliorudishwa wamepewa daktari, muuguzi na mfanyakazi wa kijamii ambaye "huandamana nao wakati wote" hadi kwao kupelekwa hospitalini.
Familia zinashauriwa kuwapa mateka "wakati kidogo" na timu za matibabu kabla ya kuunganishwa tena ili kuwaruhusu "kupumua na kuelewa kuwa wako mahali salama tena".

Chanzo cha picha, Israeli Army
"Tunaanza na vitamini, kitu kidogo cha kula na kunywa, na kisha familia," Kanali Dk Banov anasema.
Kama sehemu ya mchakato wa "kutuliza", anasema, juhudi zinafanywa kuwapa wakala wa mateka walioachiliwa kufanya maamuzi yao wenyewe, kwa maswali kama: "Je, ungependa kuoga kabla au baada ya kukutana na wazazi wako");