window.__reverb = {}; window.__reverb.__reverbLoadedPromise = new Promise((resolve, reject) => { window.__reverb.__resolveReverbLoaded = resolve; window.__reverb.__rejectReverbLoaded = reject; }); window.__reverb.__reverbTimeout = setTimeout(() => { window.__reverb.__rejectReverbLoaded(); }, 5000);

Israel yaanzisha operesheni kubwa Ukingo wa Magharibi

Takriban Wapalestina 11 wameuawa katika matukio tofauti kaskazini mwa eneo hilo.

Muhtasari

  • Afisa wa zamani wa IDF asema Iran 'inajaza' silaha katika Ukingo wa Magharibi
  • Miili tisa yafukuliwa Tanzania, mganga atuhumiwa kunyonga, kuzika hai na kuchoma moto watu
  • SpaceX yaahirisha safari ya kwanza ya binadamu kutalii angani
  • Wanajeshi wa Ukraine waliwakamata wanajeshi 594 wa Urusi Kursk - Ukraine
  • Vifaru vya Israel vyavamia mji wa Ukingo wa Magharibi
  • Papa wakaribia kutoweka Kongo-Brazzaville
  • Jeshi la Israel laanzisha operesheni kubwa Ukingo wa Magharibi
  • Namibia yazuia meli inayoshukiwa kubeba shehena ya jeshi la Israel
  • Afrika kusubiri kwa muda mrefu kupata chanjo ya mpox
  • Waendesha mashtaka waomba adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa "jaribio la mapinduzi" DRC
  • Meli iliyoshambuliwa na Wahouthi huenda inavuja mafuta - Marekani

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Wapalestina 9 wauawa huku israel ikitekeleza uvamizi katika miji ya Ukingo wa Magharibi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Takriban Wapalestina tisa wameuawa katika operesheni kubwa iliyofanywa na wanajeshi wa Israel kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, wizara ya afya ya Palestina inasema.

    Vikosi vya usalama vya Israel vilisema vimeanza "operesheni ya kukabiliana na ugaidi" huko Jenin na Tulkarm usiku kucha na kwamba hadi sasa wamewaua "magaidi watano wenye silaha kutoka angani na ardhini".

    Pia ilisema wengine wanne waliuawa katika shambulizi la anga wakati wa operesheni ya wakati mmoja katika kambi ya wakimbizi ya al-Faraa karibu na Tubas.

    Waandishi wa habari wa ndani walisema hawajaona chochote cha upeo na kiwango hiki katika Ukingo wa Magharibi tangu siku za intifada ya pili ya Wapalestina, au uasi, miongo miwili iliyopita.

  2. Na kufikia hapo tunafikia mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja

  3. Habari za hivi punde, Hamas imethibitisha kuwa wapiganaji wake sita wameuawa huko Jenin

    Kikosi cha wapiganaji wa Hamas, Brigedi ya al-Qassam, kimethibitisha katika taarifa kwamba wapiganaji wake sita wameuawa huko Jenin leo.

    Hapo awali, jeshi la Israel lilisema kuwa limewaua "magaidi watatu wenye silaha" huko Jenin katika shambulio la anga, na wengine wawili waliuawa na vikosi vya ardhini katika eneo la Jenin na Tulkarm.

  4. Afisa wa zamani wa IDF asema Iran 'inajaza' silaha katika Ukingo wa Magharibi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Conricus anasema Israel inakabiliana na "magaidi wa Kipalestina" ambao "wako karibu sana na raia wa Israel.

    Hatua ya Israel katika Ukingo wa Magharibi ni "operesheni dhidi ya silaha za Iran na mashirika ya ugaidi", msemaji wa zamani wa IDF Jonathan Conricus ameiambia kipindi cha BBC Radio 4's World.

    Conricus - ambaye sasa ni mfanyakazi katika Taasisi yenye makao yake makuu mjini Washington ya Kutetea Demokrasia - anasema vilipuzi, bunduki za kivita na bastola zinaingizwa kinyemela Ukingo wa Magharibi kupitia mpaka wa Jordan.

    "Iran inafurisha Ukingo wa Magharibi na silaha," anasema.

    Mashambulizi ya leo, anasema, ni Israel "kujilinda dhidi ya magaidi wa Kipalestina. Ni hali hatari sana kwa raia wa Israel."

  5. Miili tisa yafukuliwa Tanzania, mganga atuhumiwa kunyonga, kuzika hai na kuchoma moto watu

    .

    Chanzo cha picha, Tanzania Police

    Jeshi la Polisi nchini Tanzania linawashikilia watu wanne akiwemo mganga wa kienyeji kwa kuhusika na mauaji ya watu 10 huku vifo vyao vikihusishwa na imani za kishirikina.

    Aidha baadhi ya watu waliuwawa kwa kunyongwa, kuzikwa wakiwa hai na mwingine kuchomwa moto.

    Ilibainika kuwa miili mitatu ilikutwa imezikwa nyumbani kwa mganga huyo katika mkoa wa Singida wakati miili mingine sita ilizikwa wilayani Chemba (Dodoma) na mmoja kutupwa kwenye pori la akiba la Swangaswanga, Dodoma.

    Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime miili 9 kati ya 10 ilizikwa kwa kukalishwa kwenye shimo huku kitendo hicho kikiashiria imani za kishirikina.

    Misime alisema, matukio hayo yote yaliongozwa na mganga huyo ambapo baada ya uchunguzi kuhusu vifo vya watu watatu ambao miili yao ilifukuliwa nyumbani kwake, mganga huyo alilionyesha jeshi hilo alipozika miili mingine sita baada ya kutekeleza mauaji.

    Alibainisha kuwa waliothibitika kuuwawa baadhi walinyongwa, kuzikwa wakiwa hai na mwengine kuchomwa moto.

    Hata hivyo, miongoni mwa miili sita iliyoripotiwa kuzikwa Dodoma, miwili ilikuwa ni ya watoto waliouwawa na kuzikwa kwenye zizi la mifugo katika kipindi cha mwezi Machi na Juni mwaka jana ambapo mmoja wao alikuwa mtoto wa mganga huyo wa kienyeji.

    Jeshi hilo limesema linaendelea na uchunguzi wa mlolongo wa matukio hayo katika mkoa wa Singida na Dodoma.

    Sambamba wanafuatilia wengine wanotekeleza uhalifu kama huo.

  6. SpaceX yaahirisha safari ya kwanza ya binadamu kutalii angani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    SpaceX imeahirisha jaribio lake la kuzindua msafara unaojumuisha raia wote wenye lengo la kuzuru angani ukiwa ni kwanza kabisa kufanyika duniani.

    Misheni hiyo, inayojulikana kama Polaris Dawn, ilikuwa imeratibiwa kupaa kutoka kituo cha anga za juu cha Nasa huko Florida mapema Jumatano asubuhi.

    Saa chache kabla ya uzinduzi huo, kampuni ya Elon Musk ilisema itacheleweshwa "kwa sababu ya utabiri mbaya wa hali ya hewa" katika maeneo ambayo chombo hicho kitapitia. Haijulikani ni lini jaribio linalofuata litakuwa.

    Safari hiyo pia ilisitishwa kufuatia kuvuja heliamu kwenye laini inayounganisha mnara na roketi.

    Bilionea wa teknolojia ya Fin-tech Jared Isaacman, ambaye alianzisha kampuni ya Shift 4, ndio chanzo cha kufanyika kwa safari kama hizo.

    Analenga kuwa mwanaanga wa kwanza ambaye si mtaalamu kukamilisha ziara ya kibinafsi ya anga za juu na amepanga na kufadhili sehemu kubwa ya mradi huo na SpaceX.

    Amekataa kufichua ni kiasi gani amewekeza.Mradi wa Polaris unatumia SpaceX Dragon iliounganishwa kwenye roketi ya kampuni ya Falcon 9 kusafirisha wafanyakazi.

    Wanapanga kufikia mwinuko wa hadi kilomita 1,400 (maili 870), ambayo ikiwa itafikiwa itakuwa hatua ya juu zaidi kufikiwa na misheni yoyote tangu mpango wa Nasa wa Apollo zaidi ya miaka 50 iliyopita.

    Mfanyabiashara huyo pia ni nahodha wa safari hiyo, ambayo inashairikisha rafiki yake wa karibu na rubani mstaafu wa Jeshi la Anga la Marekani Scott Poteet, na wahandisi wawili wa SpaceX Anna Menon na Sarah Gillis.

    Wote wanne wametumikia mafunzo ya miaka miwili kwa ajili ya safari hiyo, wakitumia saa kadhaa kufanya mazoezi.

  7. Wanajeshi wa Ukraine waliwakamata wanajeshi 594 wa Urusi Kursk - Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ukraine

    Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine Oleksandr Syrsky amesema kuwa wakati wa operesheni katika Jimbo la Kursk, wanajeshi wa Ukraine waliwakamata wanajeshi 594 wa Urusi.

    Kulingana na Syrsky, Urusi ililazimika kuhamisha takriban wanajeshi 30,000 akiongezea kwamba takwimu hii inaendelea kukua.

    Wakati wa kongamano la Uhuru wa "Ukraine 2024," Syrsky alisema kuwa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine vilianzisha shambulio katika eneo la Kursk kwa sababu vikosi vya Urusi vilikuwa vikishambulia kila mara eneo la mpaka wa Ukraine"Kwa kuongezea, adui alihamisha idadi kuu ya askari na alipanga kufanya operesheni ya kukera,"

    "Shukrani kwa hatua za mafanikio za askari wetu, tumejaza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wa kubadilishana.

    Kufikia leo, wanajeshi 594 wa Jeshi la RF wametekwa katika uvamizi wa Ukraine nchini Urusi," Syrsky alisema.

    Idara ya jeshi la Urusi bado haijatoa maoni yoyote juu ya maneno ya kamanda mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine kuhusu wanajeshi wa Urusi waliokamatwa.

    Mwishoni mwa juma, gazeti la Marekani la Washington Post, likiwa limechapisha picha za video za wafungwa wa Urusi wakati wa operesheni ya Kikosi cha Wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Kursk, lilihitimisha kuwa jeshi la Ukraine lilifanikiwa kukamata angalau wanajeshi 247 wa jeshi la Urusi.

  8. Katika picha: Vifaru vya Israel vyavamia mji wa Ukingo wa Magharibi

    Baadhi ya picha kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ambapo jeshi la Israel linasema limekuwa likifanya "operesheni" ya kupambana na ugaidi.

    Tingatinga la jeshi la Israeli lilipigwa picha wakati wa uvamizi katika mji wa kaskazini wa Tulkarm asubuhi ya leo:

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Soma zaidi:

  9. Papa wakaribia kutoweka Kongo-Brazzaville

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uvuvi usiodhibitiwa wa papa unatishia usalama wa chakula hiki katika eneo la Kongo-Brazzaville huku spishi kadhaa sasa zikiwa katika hatari ya kutoweka.

    Licha ya mapishi mbadala majumbani na hata spishi za maabara, mahitaji ya papa bado yako juu barani Asia.

    Nyama ya papa ni chakula kikuu na chanzo muhimu cha protini kwa watu wanaoishi katika maeneo ya pwani ya Kongo-Brazzaville.

    Lakini idadi inayoongezeka ya meli katika bahari kuu na boti zisizodhibitiwa, zinapunguza idadi ya papa wa eneo hilo.

    Sheria za kitaifa na kimataifa hudhibiti ni kiasi gani cha samaki kinaweza kutolewa baharini na ni wapi wanaweza kuvuliwa.

    Pamoja na hayo, uvuvi usiodhibitiwa wa papa umekithiri, na kuna hatari ya kuhatarisha usalama wa chakula hiki huko Kongo-Brazzavile.

    Kundi la kimataifa la meli zilizo na zisizo na bendera limekuwa likiendesha shughuli zake katika maji haya kwa miaka mingi, na hivyo kufanya iwe vigumu kutofautisha uvuvi haramu kutokana na ule wenye leseni.

    "Wengi wao wanatoka Asia na nchi za Skandinavia, na pia kutoka nchi jirani za Senegal, Nigeria na Mali," anasema Oluwole Ojewale, ambaye anafanya kazi kama Mratibu wa Kikanda wa Kituo cha Kuchunguza Uhalifu uliopangwa kwa Afrika ya Kati.

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Kongo-Brazzaville imetenga baadhi ya maeneo kwa ajili ya uhifadhi katika jaribio la kudhibiti uvuvi.

    Hii imefanikiwa kuzuia baadhi ya shughuli haramu kuendelezwa eneo hilo.

    Lakini ufuatiliaji wa bahari kuu kwa shughuli haramu unachukua muda mwingi na gharama ni kubwa.

    Soma zaidi:

  10. Jeshi la Israel laanzisha operesheni kubwa Ukingo wa Magharibi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Takriban Wapalestina 11 wameuawa na wanajeshi wa Israel kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, maafisa wa afya wa Palestina wanasema.

    Watano waliripotiwa kuuawa katika shambulizi la anga katika kambi ya wakimbizi ya al-Far'a, na sita katika shambulio la ndege zisizo na rubani huku mapigano yenye kuhusisha silaha yakiendelea huko Jenin.

    Vikosi vya usalama vya Israel vilisema vinafanya "operesheni ya kukabiliana na ugaidi " huko Jenin na Tulkarm.

    Hii inaonekana kuwa operesheni kubwa ya Israeli, na takriban miji minne ya Palestina inalengwa kwa wakati mmoja - Jenin, Tulkarm, Nablus na Tubas.

    Ripoti za Wapalestina zinasema kuwa, barabara kuu za kuelekea Jenin zimefungwa kutokana na mapigano yenye kuhusisha silaha katika kambi ya wakimbizi ya mji huo.

    Shambulio la anga la Israel linasemekana kulenga gari katika kijiji jirani saa za alfajiri.

    Wanajeshi wa Israel wanasemekana kuingia katika hospitali moja huko Jenin na kuwazuia watu wawili huko Tulkarm.

    Uvamizi wa kijeshi wa Israel huko Nablus unaripotiwa kulenga kambi mbili za wakimbizi huko.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz alisema kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) "limekuwa likifanya kazi kwa nguvu zote tangu jana usiku katika kambi za wakimbizi za Jenin na Tulkarm ili kubomoa miundo mbinu ya kigaidi ya Iran na makundi ya Kiislamu iliyoanzishwa huko".

    Aliishutumu Iran, ambayo inaunga mkono kundi la Jihad la Palestina na Hamas, kwa kutaka kufungua kile alichokiita "mapigano ya pili" dhidi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi.

    Soma zaidi:

  11. Namibia yazuia meli inayoshukiwa kubeba shehena ya jeshi la Israel

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Meli inayoshukiwa na mamlaka ya Namibia kubeba shehena ya kijeshi iliyokusudiwa kutumiwa katika vita vinavyoendelea Gaza imezuiwa kutia nanga katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

    Waziri wa Sheria wa Namibia Yvonne Dausab aliviambia vyombo vya habari vya serikali kuwa meli hiyo ilisimamishwa kwa sababu ilikuwa na "vifaa vyenye vilipuzi vinavyopelekwa Israel".

    Meli ya MV Kathrin, ambayo ilianza safari kutoka Vietnam, ilikuwa imeomba ruhusa ya kutia nanga katika bandari ya Walvis Bay - kabla ya kuelekea kaskazini, kwenye njia inayoshukiwa kuelekea Mediterania kupitia Mlango Bahari wa Gibraltar.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalikuwa yameonya kwamba Namibia ingeweza kuhusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu kama ingeruhusu meli hiyo kutia nanga.

    Haijulikani ni kwa nini meli hiyo ilitaka kutia nanga, lakini vyombo vinavyosafiri kwa muda mrefu huwa vinasimama ili kupata mahitaji wanayohitaji kwa kipindi hicho, kupumzika, kupakua au kubeba mizigo.

    Desemba mwaka jana, jirani na mshirika wa Namibia, Afrika Kusini walifungua kesi inayoendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikidai Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

    Israel imekanusha madai ya mauaji ya halaiki na kusema kuwa "hayana msingi".

    Mzozo huo ulianza baada ya Hamas kuanzisha shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.

    Jeshi la Israel kisha lilianzisha kampeni ya kumaliza kundi la Hamas na zaidi ya watu 40,430 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

    Soma zaidi:

  12. Afrika kusubiri kwa muda mrefu kupata chanjo ya mpox

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Nchi za Afrika ambazo zimeathirika na mpox zitalazimika kusubiri muda mrefu zaidi kupata chanjo hiyo.

    Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Afrika CDC, vinasema imeweka mpango wa bara hili kukabiliana na ugonjwa huo ili upata chanjo mwezi Septemba.

    “Tunataka kuweka juhudi zetu zote sehemu moja. Afrika itakuwa na mpango mmoja wa kukabiliana na mpox na bajeti moja. Tunataka kuimarisha uwezo wa nchi kutumia chanjo hizo zitakapopatikana," Dk. Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Afrika CDC alisema.

    Hata hivyo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kitovu cha mlipuko huo, haitapokea michango iliyoahidiwa ambayo ilitarajiwa wiki hii.

    Nigeria ilipokea dozi 10,000 za chanjo ya Bavarian Nordic, Jumanne -msaada kutoka Marekani.

    Nchi hiyo ilikuwa imeanza mchakato wa kupata chanjo hizo hata kabla ya mpox kutangazwa kuwa dharura ya kiafya duniani.

    Vikwazo vya udhibiti na changamoto za manunuzi zimesababisha kuchelewa huko.

    Afrika pia inataka kupata chanjo zake kama bara na sio kama nchi moja moja.

    Soma zaidi:

  13. Waendesha mashtaka waomba adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa "jaribio la mapinduzi" DRC

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Waendesha mashtaka wa umma katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wameomba watu 50 wapewe adhabu ya kifo kwa kufanya kile ambacho jeshi linakiita "jaribio la mapinduzi" lililotokea mnamo mwezi Mei.

    Mwendesha Mashtaka wa Kijeshi Luteni Kanali Innocent Radjabu alitoa wito huo wakati wa kusikilizwa kwa kesi katika mahakama ya kijeshi ya Kinshasa.

    Hata hivyo alimtaka hakimu kumuepusha mshtakiwa mmoja kutokana na adhabu ya kifo, akisisitiza kwamba ana matatizo ya kisaikolojia.

    Miongoni mwa washtakiwa wanaokabiliwa na hukumu ya kifo ni Wamarekani watatu.

    Mnamo 19, Mei walikuwa sehemu ya kundi lililojihami ambalo lilishambulia nyumba ya aliyekuwa Waziri wa Uchumi Vitale kamerhe, ambaye sasa anahudumu kama mkuu wa Bunge la Kitaifa.

    Pia walivamia ofisi ya rais wa nchi hiyo.

    Tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo Juni 7, washtakiwa hao wamekuwa wakikabiliwa na mashtaka kuanzia "mashambulizi, ugaidi, kumiliki silaha kinyume cha sheria na zana za kivita, kujaribu kuua, kuua," miongoni mwa mengine.

    Upande wa utetezi unatarajiwa kuwasilisha kesi yake siku ya Ijumaa.

    Mwezi Machi, serikali ya DRC ilirejesha hukumu ya kifo, na hivyo kusababisha ukosoaji kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu.

    Soma zaidi:

  14. Meli iliyoshambuliwa na Wahouthi huenda inavuja mafuta - Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Meli ya mafuta iliyoshambuliwa na waasi wa Houthi wa Yemen katika Bahari ya Shamu wiki iliyopita bado inawaka moto na huenda iwaka inavuja mafuta, ikulu ya ya Marekani inasema.

    Majaribio ya kunusuru meli ya MV Sounion inayomilikiwa na Ugiriki yamezuiwa na Wahouthi, ambao wametishia mashambulizi zaidi, Pentagon inaongeza.

    Meli hiyo imebeba zaidi ya tani 150,000 - au mapipa milioni moja - ya mafuta ghafi, na kuna uwezekano ikawa na uvujaji mkubwa kuwahi kushuhudiwa miongoni mwa meli katika historia iliyorekodiwa.

    Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya Yemen, wanasema wamekuwa wakishambulia meli katika Bahari ya Shamu kwa muda wa miezi 10 kuunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

    Wameripotiwa kuzamisha meli mbili na kuua takriban wafanyikazi wawili.

    Mara nyingi wamedai kwamba wanalenga meli zenye kuhusishwa tu na Israeli, Marekani au Uingereza.

    Meli ya Sounion ilishambuliwa kwa mara ya kwanza na milio ya risasi kutoka kwa boti mbili ndogo Jumatano iliyopita, kisha ikarushiwa makombora matatu ambayo hayakujulikana ni ya aina gani, yalisababisha moto na kuiacha bila nguvu ya injini, ofisi ya Operesheni ya Biashara ya Bahari ya Uingereza ilisema.

    Wafanyakazi wake 25 waliokolewa na meli ya kivita ya Ulaya siku moja baadaye na kupelekwa Djibouti.

    Meli hiyo ya mafuta ilishambuliwa tena - Wahouthi walichapisha video inayodaiwa kuwaonyesha wakiichoma moto.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya kila siku ikiwa ni tarehe 28/08/2024